Kwanza kabisa namshukuru mwenyezi Mungu kwa  nguvu na Baraka, nawashukuru viongozi wangu wastaafu yaani  Ndugu Gambala Luchunga na John Mlyabope, viongozi na wanaumoja waliohudumu katika kamati mbalimbali za umoja wetu pamoja na wanaumoja wote wa USHIRIKIANO GROUP DSM. Kama linavyosadifu, USHIRIKIANO ndio ulitofikisha hapa na hata mimi kuchaguliwa kuongoza tasisi yetu. Aksanteni sana kwa kuniamini!

Baada ya shukrani natumia fursa hii kuwapongeza viongozi wenzangu wote waliochaguliwa kuungana na mimi katika kusukuma gurudumu la USHIRIKIANO GROUP DSM kwenda mbele zaidi ndani ya kipindi cha miaka mitatu (2023-2025). Pamoja na pongezi hizo tuna kazi ya kufanya, hivyo hakuna kulala.

Uongozi uliopita ulifanya kwa nafasi yake kubainisha mapungufu,changamoto na mitizamo hasi iliyokuwepo na kuitafutia ufumbuzi, hivyo kazi yetu ni kuanzia pale walipoishia ikiwezekana kuikamilisha.

Kipindi cha uongozi wangu nitakigawa katika vipaumbele vitatu ambavyo vitakwenda pamoja kwa namna itakavyowezekana ndani ya miaka mitatu.

Kipaumbele cha kwanza, nitaelekeza katika kamati ya maadili. Ninakusudia kuongoza taasisi inayozingatia kanuni na taratibu tulizojiwekea kwa mujibu wa katiba.

Naamini katika ushindi, hivyo ndani ya miezi sita nitakuwa nimepunguza au kuondoa kabisa ukiukwaji wa kanuni za jamii, fedha na uchumi pamoja na TeHaMa. Hili haliwezi kufanikiwa kama viongozi wa kamati hizi hawatanipa ushirikiano.

Kipaumbele cha pili, ni kuwa na taasisi yenye uchumi imara. Natarajia kuongeza bidhaa itakayoongeza pato la umoja wetu kwa kushirikiana na wataalam tulionao ndani ya umoja, naomba wanaumoja mtuunge mkono pale tutakapoleta kwenu pendekezo la aina hii.

Uwekezaji ni muhimu, hivyo nimefungua mlango kwa yeyote alie na wazo la uwekezaji asisite kutupatia, mimi pamoja na Sekretarieti tutalifanyia kazi ikiwa pamoja na kubuni vyanzo vya fedha ili kufanikisha.

Nitahakikisha gawio (Devident) kwa waliowekeza linapatikana kila mwaka ili kutoa hamasa kwa wanaumoja wengi kununua hisa kama kamati ya fedha na uchumi invyootuongoza.

Ninakusudia kutumia Tekinolojia ya Habari katika kung’amua fursa za kiuchumi, hivyo wanaumoja tunao wajibu wa kuitumia ili kupata faida katika shughuli tunazofanya ili kujipatia wateja lakini pia kufanya tovuti yetu kuwa na faida.

Baada ya kuwa na taasisi yenye nidhamu, uchumi imara na wepesi wa utumiaji katika TeHaMa nitakuwa nimejenga jamii yenye kujiamini katika kupambana na hali ngumu ya maisha, ninatamani kuona taasisi itakayomudu gharama za afya kwa kuwa na bima kwa kila mwanaumoja lakini pia kumudu bima ya mkono wa pole kwa yeyote atakaepata madhira ya msiba kwa kuondokewa na wapendwa wetu.

Nitajitahidi kuhakikisha tukio la UG DAY linaboreshwa kwa maandalizi ya muda mrefu kwani ndiyo sikukuu kubwa ya wana umoja pamoja na familia zetu.
Ni makusudio yangu kuanzisha tuzo ya mwanaumoja bora kila mwaka, kwa kushirikiana na Sekretarieti tutapendekeza vigezo na kuvileta kwenye vikao husika kuidhinishwa, hii italeta chachu ya wanaumoja kushindana kufanya vizuri na hivyo kuharakisha tija ninayoikusudia ndani ya uongozi wangu.

Kupitia kamati ya jamii, ninatarajia Jambo Ushirikiano itaendelea pale ilipoishia, hivyo wanaumoja wana fursa ya kutangaza shughuli mbalimbali za kijamii na kibiashara ili kupata wateja ndani na nje ya umoja.Ni matarajio yangu kwamba nitaungwa mkono na viongozi pamoja na wanaumoja wote.
Nina nguvu ya kujifunza kutoka kwa watangulizi wangu kama nilivyobainisha hapo awali, naomba wasiniache. Sina uwezo mkubwa wa kuyatekeleza haya lakini kwa msaada wa Mungu, viongozi wastafu, viongozi wenzangu pamoja na wanaumoja wote naamini tutashinda.

Twende na kauli mbiu hii:
“UKIPANDA KARANGA USITARAJIE KUVUNA NANASI”
USHIRIKIANO DSM – TIMIZA WAJIBU WAKO

Aksanteni sana,
Bi. Agnes Luchunga
Mwenyekiti UG-DSM 2023